Header Ads

BannerFans.com

WAZIRI WA MALIASILI, UTALII AWASILISHA BAJETI YA SH BILIONI 115


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameliomba Bunge limuidhinishie bajeti ya Sh bilioni 115.794, kwa mwaka wa fedha 2018/9, huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, ikitaka Serikali isitishe uwekaji wa vigingi vya mipaka katika maeneo ya hifadhi.

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nape Nnauye, akiwasilisha maoni ya kamati hiyo  baada ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18 kusomwa, alisema kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka baina ya wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi.

“Kamati imetoa ushauri jinsi ya kumaliza migogoro hiyo lakini bado ipo na inazidi kuongezeka.

“Hivi sasa, Serikali inaendesha zoezi la kuweka vigingi katika mipaka ya hifadhi, jambo ambalo limepingwa na wananchi na kusababisha Serikali kutumia nguvu kubwa kutekeleza zoezi hilo.

“Kamati inaona moja ya changamoto kubwa inayosababisha migogoro ni Serikali kuweka mipaka bila kuwashirikisha wananchi kwani vigingi vingine vimewekwa katika maeneo ya shule na vingine ndani ya nyumba za watu.

“Kwa hiyo, Serikali isitishe mara moja zoezi la kuweka vigingi katika mipaka ya hifadhi, Serikali ifanye tathmini mpya ya maeneo yote yaliyohifadhiwa na wananchi washirikishwe katika zoezi hilo.

“Pia, Serikali ibainishe maeneo yote ambayo bado yana sifa ya kuendelea kuhifadhiwa na ambayo hayana mgogoro ili mipaka yake ibainishwe kwa kuwashirikisha wananchi na yale ambayo yamepoteza sifa ya kuwa hifadhi yapangiwe matumizi mengine.

“Mwisho, Serikali ijipe muda wa kumaliza migogoro hiyo vinginevyo itaendelea kuunda tume na kamati mbalimbali kumaliza tatizo,” alisema Nape.
Akizungumzia ongezeko la watalii nchini, Nape alisema kamati yake hairidhishwi na jinsi Serikali inavyotoa takwimu za utalii.

“Kwa mfano, takwimu zinaonyesha idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,284,279, mwaka 2016 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

“Lakini, takwimu hizo hazichanganui ni watalii wangapi walikuja nchini kwa ajili ya mapumziko katika hifadhi zetu, jambo ambalo halitoi picha halisi ya mwenendo wa ukuaji wa sekta hii.
“Pamoja na hayo, Machi 17, mwaka 2016, Serikali ilisitisha biashara ya wanyamapori hai nje ya nchi na kusababisha hali ya taharuki kwa wafanyabiashara hao.

“Chama cha Wasafirishaji Wanyama Hai Nje ya Nchi (TWEA), kilitoa malalamiko yake kwamba wakati Serikali ikisitisha biashara hiyo, wafanyabiashara hao walikuwa wamechukua mikopo benki, walikuwa wamelipia leseni na tozo mbalimbali za Serikali na walikuwa wakiwatunza wanyamapori waliokuwa wamewakamata kwa gharama kubwa wakisubiri kuwasafirisha nje.

No comments

Powered by Blogger.