MRITHI WA KINANA APATIKANA, YULE ALIYECHUNGUZA MALI CCM

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Ma
pinduzi (NEC), imemteua Dk. Bashiru Ali kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tawala akirithi nafasi ya Abdulrahman Kinana.
Dk. Bashiru ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza mali za CCM anachukua nafasi hiyo na kuwa Katibu Mkuu wanane wa chama hicho tawala nchini.
Uteuzi huo wa Muhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), umekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli kuridhia barua ya kujiuzulu Kinana mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jioni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema NEC imeridhia uteuzi wa kiongozi huyo.
Polepole alisema katika taarifa yake kuwa NEC imeteuwa makatibu wapya wa Jumuiya za chama ambapo, Raymond Mangwala ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), ambapo hadi anapata uteuzi alikuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Pamoja na hali hiyo pia ni moja ya vijana waliokulia na mwenye kujua silka na hulka za UVCCM kwa kushika nafasi mbalimbali.
Nafasi alizopata kushika ni pamoja na Mwenyekiti wa Chipukizi Taifa, Katibu wa UVCCM Wilaya za Kyela na mikoa ya Dodoma na Ruvuma pamoja na kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya.
Pia ilitaja wengine walioteuliwa Mwalimu Queen Mlozi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, huku Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Erasto Sima ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba.
Post a Comment