Yanga yapeleka Barua yakujitoa Rasmi michuano ya Kagame cup
YANGA SC imeandika barua ya kujitoa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ikiwa ni siku tatu tu tangu kutajwa kwa ratiba, ikiwa imepangwa Kundi A na mahasimu wao, Simba SC.
Akizungumza na wandishii leo mjini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga, Dissmas Ten amesema kwamba wamepeleka barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujitoa kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano.
“Ni kweli hatutashiriki mashindano ya Kagame Cup kutokana na ratiba kuwa ngumu kwa upande wetu, kumekuwa na msongamano wa mashindano baada ya kumalizika kwa ligi tumeenda Kenya kwenye michuano ya SportSpesa Super Cup, tumerudi majuzi tu hapa,”
“Pia tuna mechi nyingine ya Kombe la Shirikisho Afrika tutakayocheza nchini Kenya Juni 16 mwaka huu dhidi ya Gor Mahia, hivyo ukiangalia msongamano huo hata wachezaji wetu watakosa muda wa kupumzika, hivyo tumeona ni bora kutoshiriki mashindano hayo ili kuwapa muda wachezaji wetu ili waweze kujiandaa na mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika,”amesema Ten.
Juni 5, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetaja ratifa ya Kombe la Kagame, michuano inayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu mjini Dar es Salaam na vigogo wa soka Tanzania, Simba SC na Yanga SC watamenyana Julai 5, mwaka huu katika mechi ya Kundi C.
Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwamba pamoja na Simba na Yanga, timu nyingine katika Kundi hilo ni Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.
Post a Comment